Alhamisi, 13 Machi 2014

WAZEE 11OO WANUFAIKA NA PENSHENI MULEBA

 Moses Augustine,Muleba,13,March 2014

WAKATI serikali ikiwa bado na kigugumizi cha kuwalipa pensheni wazee nchini,Shirika lisilo la kiserikali la Kwa wazee lililopo wilayani Muleba Mkoani Kagera limeanzisha mpango wa kuwalipa pensheni wazee 1,100 wakiwemo waliotelekezwa na familia zao.

Wazee hao wenye umri wa kuanzia miaka 60 wanalipwa kila mwezi kiasi cha shilingi 12,000 pamoja na shilingi 7,000 kwa wajukuu tegemezi wanaolelewa na wazee kutokana na wazazi wao kukimbilia mijini na wengine kufariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mratibu wa shirika hilo,Lidiah Lugazia,alisema uamuzi huo umetokana na shirika lake kubaini kuwa wazee wengi nchini wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha licha ya kuwa na mchango mkubwa kwa taifa.

Katika wilaya ya muleba utafiti unaonyesha kuwa wazee wengi wanaishi katika mazingira magumu huku wakilea wajukuu baada ya wazazi wao kufariki kwa ugonjwa wa Ukimwi.

Kwa mujibu wa mshauri mkuu wa shirika hilo kutoka nchini Switzerland,Dk. Kurt Madoerin,kwa kutambua umuhimu wa wazee duniani,nchi yake imelazimika kushirikiana na shirika la Kwa wazee la wilayani Muleba kuhakikisha wazee wanapata misaada ya kijamii na kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kusababisha kufa mapema.

Alisema zaidi ya shilingi milioni 500 zimetolewa kwa shirika hilo ili kusaidia kuwalipa pesheni ya kila mwezi wazee 1,100 kwa kipindi cha mwaka mmoja pamoja na watoto yatima sanjari na kuwasomesha elimu ya msingi na sekondari.

Hata hivyo alionyesha kusikitishwa na imani potofu kwa jamii ya kitanzania kuwatuhumu wazee kuwa ni wachawi badala ya kuwathamini na kuwatunza ili kulinda mila na desturi zilizo njema kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Mzee Hezron Malungu(75),Sabina John (81) na Regna Apolinari,waliitupia lawama serikali kushindwa kuwalipa pensheni wazee waliolitumikia taifa kwa kipindi chao chote katika nyanja mbalimbali na kwamba inasikitisha kuona asasi ya kiraia imeweza kuwasaidia baada ya kuanza kuwalipa 12,000 kila mwezi.

"Inasikitisha sana pale tunapopigwa danadana na serikali yetu juu ya kutulipa pensheni....matamko ya ahadi yamekuwa mengi yasiyokuwa na utekelezaji wowote....tumeanza kulipwa na shirika hili... hivi sasa tunafurahia maisha yetu hata kama ni kukopeshwa unga dukani muuzaji anakubali akiamini utamlipa mwisho wa mwezi baada ya kupokea" alisema Selestina Paulo.

Mkuu wa mkoa wa Kagera,Fabian Masawe,mbali na kuipongeza asasi hiyo,amedai kuwa wazee wanapaswa kuvuta subira juu ya malipo ya pensheni kwa kuwa tayari kuna matamko mbalimbali ya serikali ambayo yanadhihilisha kushughulikiwa kwa suala hilo.

Hata hivyo alitoa wito kwa vijana kujiandalia mazingira mazuri ya uzeeni badala ya kufuja mali walizonazo ambazo baadaye hugeuka majuto kipindi wanapozeeka na kukosa nguvu za kuzalisha mali.

                                    Mwisho.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni