Moses Augustine,Muleba,13,March 2014
WAKATI
serikali ikiwa bado na kigugumizi cha kuwalipa pensheni wazee
nchini,Shirika lisilo la kiserikali la Kwa wazee lililopo wilayani
Muleba Mkoani Kagera limeanzisha mpango wa kuwalipa pensheni wazee 1,100
wakiwemo waliotelekezwa na familia zao.
Wazee
hao wenye umri wa kuanzia miaka 60 wanalipwa kila mwezi kiasi cha
shilingi 12,000 pamoja na shilingi 7,000 kwa wajukuu tegemezi wanaolelewa
na wazee kutokana na wazazi wao kukimbilia mijini na wengine kufariki
kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mratibu wa shirika hilo,Lidiah Lugazia,alisema uamuzi huo
umetokana na shirika lake kubaini kuwa wazee wengi nchini wamekuwa
wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha licha ya kuwa na mchango mkubwa kwa
taifa.
Katika
wilaya ya muleba utafiti unaonyesha kuwa wazee wengi wanaishi katika
mazingira magumu huku wakilea wajukuu baada ya wazazi wao kufariki kwa
ugonjwa wa Ukimwi.
Kwa
mujibu wa mshauri mkuu wa shirika hilo kutoka nchini Switzerland,Dk.
Kurt Madoerin,kwa kutambua umuhimu wa wazee duniani,nchi yake
imelazimika kushirikiana na shirika la Kwa wazee la wilayani Muleba
kuhakikisha wazee wanapata misaada ya kijamii na kupunguza msongo wa
mawazo unaoweza kusababisha kufa mapema.
Alisema
zaidi ya shilingi milioni 500 zimetolewa kwa shirika hilo ili kusaidia
kuwalipa pesheni ya kila mwezi wazee 1,100 kwa kipindi cha mwaka mmoja
pamoja na watoto yatima sanjari na kuwasomesha elimu ya msingi na
sekondari.
Hata
hivyo alionyesha kusikitishwa na imani potofu kwa jamii ya kitanzania
kuwatuhumu wazee kuwa ni wachawi badala ya kuwathamini na kuwatunza ili
kulinda mila na desturi zilizo njema kwa manufaa ya sasa na baadaye.
Mzee
Hezron Malungu(75),Sabina John (81) na Regna Apolinari,waliitupia
lawama serikali kushindwa kuwalipa pensheni wazee waliolitumikia taifa
kwa kipindi chao chote katika nyanja mbalimbali na kwamba inasikitisha
kuona asasi ya kiraia imeweza kuwasaidia baada ya kuanza kuwalipa 12,000
kila mwezi.
"Inasikitisha
sana pale tunapopigwa danadana na serikali yetu juu ya kutulipa
pensheni....matamko ya ahadi yamekuwa mengi yasiyokuwa na utekelezaji
wowote....tumeanza kulipwa na shirika hili... hivi sasa tunafurahia
maisha yetu hata kama ni kukopeshwa unga dukani muuzaji anakubali
akiamini utamlipa mwisho wa mwezi baada ya kupokea" alisema Selestina
Paulo.
Mkuu
wa mkoa wa Kagera,Fabian Masawe,mbali na kuipongeza asasi hiyo,amedai
kuwa wazee wanapaswa kuvuta subira juu ya malipo ya pensheni kwa kuwa
tayari kuna matamko mbalimbali ya serikali ambayo yanadhihilisha
kushughulikiwa kwa suala hilo.
Hata
hivyo alitoa wito kwa vijana kujiandalia mazingira mazuri ya uzeeni
badala ya kufuja mali walizonazo ambazo baadaye hugeuka majuto kipindi
wanapozeeka na kukosa nguvu za kuzalisha mali.
Mwisho.