Jumanne, 19 Agosti 2014

DK. EDMUND MNDOLWA: MSIWABUGHUDHI VIONGOZI WALIOPO MADARAKANI WAACHENI WACHAPE KAZI

Dotto Mwaibale

WANACHAMA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wametakiwa kuacha kuwabugudhi viongozi waliopo madarakani kwa kuchaguliwa waendelee kuchapa kazi badala ya kuanza kuzihitaji nafasi zao kabla ya wakati.

Mwito huo umetolewa na Mjumbe wa Halmshauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Chama hicho wilaya ya Korogwe mkoani Tanga Dk.Edmund Mndolwa wakati akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dar es Salaam leo.

"Wito wangu kwa wanachama wenzangu wenye lengo la kutaka kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika chama chetu wasianze kutamka nia ya kuwania nafasi hizo kabla ya wakati kwani kufanya hivyo ni kuwapunguzia kasi ya utendaji  viongozi waliopo madarakani.

Mndolwa alisema mtu anapotokea kuanza kuonesha nia kwa mfano wa kugombea ubunge katika eneo fulani kunamfanya mbunge aliopo katika eneo hilo kuacha kufanya shughuli za kuwatumikia wananchi badala yake anaanza kutumia muda mwingi wa kupambana na mtu huyo anayetaka kugombea kwenye jimbo husika.

Katika hatua nyingine Mndolwa amewataka watanzania kuendelea na mchakato wa Bunge la Katiba kwani ndio mahitaji yao badala ya kusitisha Bunge la Katiba linaloendelea mkoani Dodoma.

"Kwa mtazamu wangu ni vizuri mchakato wa bunge hilo ukaendelea kwani ndio mahitaji ya watanzania waliowengi kukomea njiani ni kupoteza mabilioni ya fedha za wananchi kutoka na vikao vinavyoendelea kufanyika" alisema Mndolwa,.

Mndolwa alisema hivi sasa yupo katika ziara ya kutembelea mashina na matawi ya CCM wilayani humo kwa ajili ya kuimarisha uhai wa chama na kujua changamoto mbalimbali zilizopo ili kuziwasilisha ngazi ya juu kwa hatua ya utekelezaji.

SIMTANK YAKABIDHI ZAWADI KWA WATEJA WAKE




Jumapili, 17 Agosti 2014

WAMAHIAJI HARAMU 21 WAKAMATWA NJOMBE WAKIPENYA KWENDA NCHI ZA KUSINI MWA TANZANIA

Hawa  ni  raia  wa  Ephiopia ambao  walikamatwa  Makambako  Njombe  jana
hapa  wakipata  chai  baada ya kukamatwa
Hivi  ndivyo  walivyokuwa  wakiishi katika  lori  hilo
Hili  ndilo  lori  lililokuwa  likiwasafirisha na  dereva  wake  kukimbia
Ofisa uhamiaji  Njombe  akiwapa  chai wahamiaji hao
 Chanzo francis Godwin Blog

Alhamisi, 13 Machi 2014

WAZEE 11OO WANUFAIKA NA PENSHENI MULEBA

 Moses Augustine,Muleba,13,March 2014

WAKATI serikali ikiwa bado na kigugumizi cha kuwalipa pensheni wazee nchini,Shirika lisilo la kiserikali la Kwa wazee lililopo wilayani Muleba Mkoani Kagera limeanzisha mpango wa kuwalipa pensheni wazee 1,100 wakiwemo waliotelekezwa na familia zao.

Wazee hao wenye umri wa kuanzia miaka 60 wanalipwa kila mwezi kiasi cha shilingi 12,000 pamoja na shilingi 7,000 kwa wajukuu tegemezi wanaolelewa na wazee kutokana na wazazi wao kukimbilia mijini na wengine kufariki kutokana na ugonjwa wa Ukimwi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mratibu wa shirika hilo,Lidiah Lugazia,alisema uamuzi huo umetokana na shirika lake kubaini kuwa wazee wengi nchini wamekuwa wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha licha ya kuwa na mchango mkubwa kwa taifa.

Katika wilaya ya muleba utafiti unaonyesha kuwa wazee wengi wanaishi katika mazingira magumu huku wakilea wajukuu baada ya wazazi wao kufariki kwa ugonjwa wa Ukimwi.

Kwa mujibu wa mshauri mkuu wa shirika hilo kutoka nchini Switzerland,Dk. Kurt Madoerin,kwa kutambua umuhimu wa wazee duniani,nchi yake imelazimika kushirikiana na shirika la Kwa wazee la wilayani Muleba kuhakikisha wazee wanapata misaada ya kijamii na kupunguza msongo wa mawazo unaoweza kusababisha kufa mapema.

Alisema zaidi ya shilingi milioni 500 zimetolewa kwa shirika hilo ili kusaidia kuwalipa pesheni ya kila mwezi wazee 1,100 kwa kipindi cha mwaka mmoja pamoja na watoto yatima sanjari na kuwasomesha elimu ya msingi na sekondari.

Hata hivyo alionyesha kusikitishwa na imani potofu kwa jamii ya kitanzania kuwatuhumu wazee kuwa ni wachawi badala ya kuwathamini na kuwatunza ili kulinda mila na desturi zilizo njema kwa manufaa ya sasa na baadaye.

Mzee Hezron Malungu(75),Sabina John (81) na Regna Apolinari,waliitupia lawama serikali kushindwa kuwalipa pensheni wazee waliolitumikia taifa kwa kipindi chao chote katika nyanja mbalimbali na kwamba inasikitisha kuona asasi ya kiraia imeweza kuwasaidia baada ya kuanza kuwalipa 12,000 kila mwezi.

"Inasikitisha sana pale tunapopigwa danadana na serikali yetu juu ya kutulipa pensheni....matamko ya ahadi yamekuwa mengi yasiyokuwa na utekelezaji wowote....tumeanza kulipwa na shirika hili... hivi sasa tunafurahia maisha yetu hata kama ni kukopeshwa unga dukani muuzaji anakubali akiamini utamlipa mwisho wa mwezi baada ya kupokea" alisema Selestina Paulo.

Mkuu wa mkoa wa Kagera,Fabian Masawe,mbali na kuipongeza asasi hiyo,amedai kuwa wazee wanapaswa kuvuta subira juu ya malipo ya pensheni kwa kuwa tayari kuna matamko mbalimbali ya serikali ambayo yanadhihilisha kushughulikiwa kwa suala hilo.

Hata hivyo alitoa wito kwa vijana kujiandalia mazingira mazuri ya uzeeni badala ya kufuja mali walizonazo ambazo baadaye hugeuka majuto kipindi wanapozeeka na kukosa nguvu za kuzalisha mali.

                                    Mwisho.

WATATU WASHIKILIWA NA JESHI LA POLISI KAGERA

 Moses Augustine ,Muleba,13,3,2014


JESHI la polisi mkoani Kagera linawashikilia watu watatu akiwemo mchungaji wa kanisa la Chochea moto, Elmes Fabian,kwa tuhuma za kufanya uharifu, kufyeka mashamba ya migomba na kuvunja nyumba 3 za wakazi wa kijiji cha Kishulo wilayani Muleba wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.

Tukio hilo limesababisha wananchi zaidi ya 12 wakiwemo watoto na wanafunzi wa shule za msingi kukosa makazi huku wazazi wao wakilazimika kukimbilia kwenye taasisi ya kusaidia wazee na yatima ya "Kwa Wazee" iliyopo kata ya Nshamba ili kupata hifadhi ya muda.

Kamanda wa polisi mkoa wa Kagera, George Mayunga,amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa watu watatu akiwemo mchungaji wa kanisa la Chochea moto(Emba Omulilo) wanashikiliwa kwa kosa la kuchochea vurugu,kudhuru miili na kuharibu mali kinyume cha sheria.

Amesema uchunguzi wa jeshi hilo umebaini baadhi ya wananchi wakiwemo watoto wa watuhumiwa hao wa ushirikina walifanya ukatili huo wakishirikiana na baadhi ya wananchi waliokuwa na lengo la kuwaua wazee wa familia hizo.

Kamanda Mayunga amewataja walionusurika kuuawa kuwa ni Fabian Albert na mkewe Gaudensia Fabian,Methodia Leonard na Geogina Kayonga wote wakazi wa kijiji cha Kashulo wilayani humo mkoani kagera.

Mchungaji wa kanisa la Chochea Moto(Emba Omulilo) anadaiwa kuwahubiri waumini wake kuwa anauwezo mkubwa wa kuwabaini wachawi ambao wamekuwa wakisumbua kijijini humo kabla ya kuanza kuwataja kwa majina.

Hatua hiyo ilionekana kupokelewa kwa hisia kali na waumini wake wakiwemo watoto wa watuhumiwa, hivyo kuungana na wananchi wengine kwenda kuharibu mali na kuwadhuru wazee hao kwa mapanga.

Mratibu wa shirika lisilokuwa la kiserikali la "Kwa Wazee" Lydiah Lugazia,amesema kutokana na ukatili huo kwa wazee hao wamelazimika kuwachukua na kuwahifadhi kwa muda ili kunusuru maisha yao kufuatia wananchi kutaka kuwaua kwa imani potofu za kishirikina.

Aidha msaada huo ni wa siku chache huku akiitaka serikali kuweka mazingira mazuri kwa walioathiliwa na ukatili huo kutafuta ufumbuzi wa kuwalejesha katika maneo yao na kuimalisha ulinzi ili waendelee na shughuli zao za uzalishaji mali.

Kwa Upande wake Ofisa miradi wa asasi hiyo,Edmund Revelian,ameiomba serikali kuacha kusajili makanisa kinyemela kwa kuwa baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakichochea vurugu kwa jamii kutokana na maslahi yao binafsi.

Kadhalika ameonyesha kushangazwa na jamii kuamini sana imani za kishirikina ambazo kwa kiwango kikubwa zimekuwa zikiwakumba wananchi maskini,huku wengine wakitumia nafasi hizo kutaka kupokonya mali za wengine iwapo watafanikiwa kuwatimua kutoka kijijini humo.

Kwa upande wao watuhumiwa wa vitendo hivyo vya kishirikina walipoulizwa na gazeti hili kuhusiana na tuhuma dhidi yao walikanusha vikali na kudai huo ni mpango kabambe ambao umesukwa kitambo na watoto wao ili wafanikiwe kutwaa mashamba na nyumba za wazazi wao.

Wamesema kabla ya tukio hilo,watoto wao wamekuwa wakiwatishia kuwaua iwapo hawatakuwa tayari kuwapa mashamba iliwauze na kupata pesa za kufanya mambo yao.

Kutokana na hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Kagera,Kanali mstaafu Fabian Masawe,ametumia nafasi hiyo kuwaonya wananchi wote mkoani humo ambao wamekuwa na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kwamba wanapaswa kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama iwapo kuna mtu wanamshuku kuwa siyo mwema kwa jamii.

Kadhalika amewataka vijana wanaoendesha vitendo hivyo kutambua kuwa kuzeeka siyo kuwa mchawi na kwamba hata wao ipo siku watazeeka kwa kuwa huo ni mpango wa Mungu na badala yake wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili waboreshe maisha yao kuliko kutegemea mali za wazazi wao.

                                        Mwisho.