Moses Augustine ,Muleba,13,3,2014
JESHI
la polisi mkoani Kagera linawashikilia watu watatu akiwemo mchungaji wa
kanisa la Chochea moto, Elmes Fabian,kwa tuhuma za kufanya uharifu,
kufyeka mashamba ya migomba na kuvunja nyumba 3 za wakazi wa kijiji cha
Kishulo wilayani Muleba wakiwatuhumu kuwa ni wachawi.
Tukio
hilo limesababisha wananchi zaidi ya 12 wakiwemo watoto na wanafunzi wa
shule za msingi kukosa makazi huku wazazi wao wakilazimika kukimbilia
kwenye taasisi ya kusaidia wazee na yatima ya "Kwa Wazee" iliyopo kata
ya Nshamba ili kupata hifadhi ya muda.
Kamanda
wa polisi mkoa wa Kagera, George Mayunga,amethibitisha kuwepo kwa tukio
hilo na kudai kuwa watu watatu akiwemo mchungaji wa kanisa la Chochea
moto(Emba Omulilo) wanashikiliwa kwa kosa la kuchochea vurugu,kudhuru
miili na kuharibu mali kinyume cha sheria.
Amesema
uchunguzi wa jeshi hilo umebaini baadhi ya wananchi wakiwemo watoto wa
watuhumiwa hao wa ushirikina walifanya ukatili huo wakishirikiana na
baadhi ya wananchi waliokuwa na lengo la kuwaua wazee wa familia hizo.
Kamanda
Mayunga amewataja walionusurika kuuawa kuwa ni Fabian Albert na mkewe
Gaudensia Fabian,Methodia Leonard na Geogina Kayonga wote wakazi wa
kijiji cha Kashulo wilayani humo mkoani kagera.
Mchungaji
wa kanisa la Chochea Moto(Emba Omulilo) anadaiwa kuwahubiri waumini
wake kuwa anauwezo mkubwa wa kuwabaini wachawi ambao wamekuwa wakisumbua
kijijini humo kabla ya kuanza kuwataja kwa majina.
Hatua
hiyo ilionekana kupokelewa kwa hisia kali na waumini wake wakiwemo
watoto wa watuhumiwa, hivyo kuungana na wananchi wengine kwenda kuharibu
mali na kuwadhuru wazee hao kwa mapanga.
Mratibu
wa shirika lisilokuwa la kiserikali la "Kwa Wazee" Lydiah
Lugazia,amesema kutokana na ukatili huo kwa wazee hao wamelazimika
kuwachukua na kuwahifadhi kwa muda ili kunusuru maisha yao kufuatia
wananchi kutaka kuwaua kwa imani potofu za kishirikina.
Aidha
msaada huo ni wa siku chache huku akiitaka serikali kuweka mazingira
mazuri kwa walioathiliwa na ukatili huo kutafuta ufumbuzi wa kuwalejesha
katika maneo yao na kuimalisha ulinzi ili waendelee na shughuli zao za
uzalishaji mali.
Kwa
Upande wake Ofisa miradi wa asasi hiyo,Edmund Revelian,ameiomba
serikali kuacha kusajili makanisa kinyemela kwa kuwa baadhi ya viongozi
wa dini wamekuwa wakichochea vurugu kwa jamii kutokana na maslahi yao
binafsi.
Kadhalika
ameonyesha kushangazwa na jamii kuamini sana imani za kishirikina
ambazo kwa kiwango kikubwa zimekuwa zikiwakumba wananchi maskini,huku
wengine wakitumia nafasi hizo kutaka kupokonya mali za wengine iwapo
watafanikiwa kuwatimua kutoka kijijini humo.
Kwa
upande wao watuhumiwa wa vitendo hivyo vya kishirikina walipoulizwa na
gazeti hili kuhusiana na tuhuma dhidi yao walikanusha vikali na kudai
huo ni mpango kabambe ambao umesukwa kitambo na watoto wao ili
wafanikiwe kutwaa mashamba na nyumba za wazazi wao.
Wamesema
kabla ya tukio hilo,watoto wao wamekuwa wakiwatishia kuwaua iwapo
hawatakuwa tayari kuwapa mashamba iliwauze na kupata pesa za kufanya
mambo yao.
Kutokana
na hali hiyo Mkuu wa mkoa wa Kagera,Kanali mstaafu Fabian
Masawe,ametumia nafasi hiyo kuwaonya wananchi wote mkoani humo ambao
wamekuwa na tabia ya kujichukulia sheria mkononi na kwamba wanapaswa
kutoa taarifa kwenye vyombo vya usalama iwapo kuna mtu wanamshuku kuwa
siyo mwema kwa jamii.
Kadhalika
amewataka vijana wanaoendesha vitendo hivyo kutambua kuwa kuzeeka siyo
kuwa mchawi na kwamba hata wao ipo siku watazeeka kwa kuwa huo ni mpango
wa Mungu na badala yake wanapaswa kufanya kazi kwa bidii ili waboreshe
maisha yao kuliko kutegemea mali za wazazi wao.
Mwisho.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni